Marafiki zangu kadhaa wameanza kunihoji kuhusu kukosekana kwa zile makala zinazochokoza ubongo na hisia, kwasababu wanajua fika nasoma na kufuatilia habari za nchi yetu Tanzania kila kukicha.
Kitu ambacho wanasahau ni kuwa kukumbushana na kujadili mambo yanayotugusa moja kwa moja au njia nyingine ni jukumu letu sote — mtu mmoja mmoja. Kwasababu tunajifunza mengi zaidi tunapofanya midahalo na kusikiliza hoja zinazokinzana. Sasa, tunapokosea mara nyingi ni kusubiri fulani atupe mtazamo wake kwanza, kisha sisi ndio tunaunga tela na kusema, “Makala nzuri kijana!” Au, “It was a very good read.” Good f***ing read? Yaani, mi’ najipinda kufanya utafiti wa hapa na pale na kutulia kuhakikisha makala zinakuwa na mtiririko mzuri, halafu watu wanakuja na maoni ya kigoigoi?
Wakati mwingine naona ni kama kejeli tu, kwasababu hakuna mtu anayejua kila kitu! Pia, binadamu tuna hulka ya kuwa na mitazamo tofauti; tunajenga hoja kwa kutumia fikra tofauti na ni kawaida kuwa na hoja zinazokinzana. Mbona sijawahi kusikia mtu na mke wake wamehairisha fungate baada ya kugundua mume ni shabiki wa Yanga na mamaa ni shabiki wa Simba. Mlio kwenye ndoa, tafadhali, nifungueni macho.
Ndio, tuna waandishi maarufu kama Jenerali Ulimwengu ambaye ana upeo wa hali ya juu. Ila nikikubaliana naye tu bila hata kuacha kwanza hoja zake ziogelee kwenye bahari ya fikra zangu, basi nitakuwa nawatukana kina Socrates na Aristotle matusi ya nguoni.
Huwa najiuliza, hivi Socrates na Aristotle wakifufuka leo, halafu tuwaoneshe “midahalo” yetu — sisi Watanzania — je, watafanya nini? Namuona Socrates akiomba kamba ya katani na stuli… halafu anatoka mkuku kuelekea msituni, stuli kichwani, anapiga mayowe huku akitengeneza kitanzi!
Yule Mwanakijiji wa Jamii Forums alishawahi kusema kwamba Bongo tunahitaji kuwa na somo la logic kwenye mitaala yetu. Unaweza ukasema jamaa alikuwa anaota. Angalia, mshua mwenyewe tu alisepa mdahalo mwaka jana! Mshua alipaswa kuwa mfano wa kuigwa…
Wakati bado unang’aang’aa macho na kujiuliza kwanini mwandishi ameamua kuiita hii makala “Mbwa wa Pavlov”, turudi kwenye siasa na muelekeo wa nchi yetu. Tanzania.
Ili kuhakikisha fikra zangu hazichukuliwi msukule na wapuuzi, nimeamua kuupa ubongo wangu likizo za hapa na pale. Kitu ambacho nakifanya ni kutosoma habari na makala zinazojadili muelekeo wa Tanzania kwa kipindi fulani. Kwanini? Jibu ni rahisi: mtiririko unatabirika; majina tu ndio yanabadilika. Niliona nifanye hivyo kwasababu kuna kipindi nilijikuta naanza kuamsha hisia fulani kabla ya hata kumaliza kusoma vichwa vya habari!
Tukatae kutoa udenda tunaposikia kelele za kengele tu. Tunapaswa kujua kengele ipi inaasharia msosi uko tayari, wapi tunapaswa kubweka, wapi tunatakiwa kumtoa dima mwizi na wapi tunapopaswa kung’ata! Kama bado hunielewi basi kubali wewe ni Mbwa wa Pavlov. Na hiyo sio sifa.
Leo tumeamka na kukuta habari ya watoto wawili waliomuua mwenzao wa miaka miwili. Wengi watashtuka sana na kutoa maoni yao juu ya jambo hili. Lakini, hebu tajaribu kulichunguza hili tukio kwa kurunzi kubwa zaidi ili tuhakikishe halitokei tena.
Je, mazingira na mazingara ya jamii yetu yanaweza kusababisha matukio kama haya? Watoto wanazaliwa wachoyo? Au wezi? Nini husababisha watoto kupata ‘kiburi’ cha kumpiga mwenzao na mawe hadi kufa?
Unakumbuka, mara ngapi watu wamejaribu kuanzisha mijadala kuhusu mauaji ya vibaka wanapokamatwa na wananchi wenye “hasira kali”? Akili za watoto zinafyonza kila kitu wanachoona na haya ndio matokeo yake.
Mbwa wa Pavlov wataanza kutafuta visingizio badala ya kutafuta njia za kutatua tatizo. Hawaoni miaka kumi, ishirini au thelathini baadae. Kengele zimepigwa sana tu, ila wengi wanadhani kila kengele huashiria chakula kiko njiani!
Mengi sana yametokea kwenye miezi miwili-mitatu iliyopita, ambayo yanafanya ujiulize maswali lukuki…